SUKARI iliyoagizwa na serikali kutoka nje kwa ajili ya kujazia uhaba wa sukari kwa mfumo rasmi, imewasili nchini na tani takribani 12,000 zitaanza kusambazwa leo katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna upungufu wa sukari kwa mfumo rasmi, lakini serikali ilichukua hatua ya kuhakikisha inapatikana sukari kufidia uhaba huo na kuwa suala la sukari lisionekane kuwa tatizo kubwa.
“Sukari ipo lakini sio kwa kiwango halisi kinachopaswa kuwepo, lakini kama wafanyabiashara wangefanya biashara ya kuuza sukari kwa utaratibu mzuri uliowekwa wangekwenda sambamba na mfumo rasmi wa kuagiza sukari kujazia uhaba uliopo,” alisema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kiuhalisia zinahitajika tani 420,000 lakini uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha ni tani 320,000 kwa hiyo kuna upungufu wa tani 100000 na ndio maana serikali imelazimika kuagiza nje kufidia upungufu huo.
Alisema mkakati wa serikali ni kuimarisha viwanda vyake vya kuzalisha sukari, sambamba na kudhibiti sukari ya nje kuvifanya viwanda vya ndani vinakuwa na uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha pamoja na kuhamasisha wananchi kuwa na utamaduni wa kutumia bidhaa yao ya ndani.
Tani 11,957 zatua “Lakini tumechukua hatua kwa sasa kuagiza sukari nje tani 70,000 kujazia upungufu huo kwa sababu kwa sasa hivi viwanda vyetu havina uwezo wa kuzalisha sukari ya kutosha, vipo vingine vinahitaji kuboreshwa ama kukarabatiwa kabla havijaanza kazi,” alieleza Waziri Mkuu.
Alisema katika kujazia upungufu huo, tayari serikali imeingiza tani 11,957 ambazo zimeshawasili na zitaanza kusambazwa leo kikanda pamoja na kiwango cha tani kwenye mabano mikoa ya Kaskazini (tani 2,000), Kanda ya Ziwa (tani 3,000), Kusini (2,000), Nyanda za Juu Kusini (2,000) na Kanda ya Kati (2,000).
Alisema tani nyingine 24,000 za sukari, zinatarajiwa kuwasili Ijumaa hii na kwamba hadi kukamilisha taratibu na kutoka bandarini itakuwa kama Jumapili, hivyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu ijayo.
Waziri Mkuu alisema pia tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi ujao na kwamba serikali inaamini upungufu uliokuwepo, utakuwa umejaziliziwa vizuri wakati ikitarajia ifikapo mwezi Julai viwanda vya ndani vitakuwa katika hali nzuri ya kuanza uzalishaji.
“Watanzania wasiwe na wasiwasi kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache. Rais amekuwa makini kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na uhaba huo ikiwa ni pamoja na kuagiza waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe,” alisema
0 comments:
Post a Comment